Alhamisi, 3 Aprili 2014

MABO YANAYOWEZA KUBORESHA UKARIBU/ URAFIKI BAINAYETU NA WATOTO




1.         Kuwakubali na kuwapenda watoto (Appreciation)
Ni ngumu kabisa kuwa karibu na watoto na kutafuta kukubalika nao pasipo kwanza kuwakubali.  Mawasiliano yako na wao yanatakiwa kuwa ya kiwango cha juu kuliko yale unayofanya na watu wazima.  Kama ni mzazi, tamani au tafuta kuutumia muda unapokuwa na watoto vizuri.  Wape muda na wewe kadri inavyowezekana.

Shiriki nao katika baadhi ya yale wanayoyafanya.  Washirikishe pia katika yale unayodhani watapenda kuona ukiyafanya.  Usiwaangalie tu au kuwaacha wakutazame ukifanya.  Kumpakata mtoto wakati wa hadithi ni mfano wa kushiriki nae.  Hii hujenga mahusiano mazuri sana kwao.


2.         Kuwa tayari kutumia nguvu zetu au nishati yetu ya mwili kwa ajili yao
Watoto huwa na nishati au nguvu nyingi katika vile wanavyovifanya.  Hali kadhalika mtu anayetamani kuwa karibu nao ni lazima awe tayari kutumia nguvu zake katika kushiriki nao.  Mfano, watapenda kukimbizana, watapenda kuruka, au kutembea haraka na michezo mingine mingi.

3.         Kuwa na hali nzuri ya utu (Sense of humor)
Hali hii huwafanya watoto kukuona wewe ni sawa nao.  Watoto hupenda sana pale unapokuwa tayari kucheka na kuwa na hisia kama walizonazo.
Najua unahitaji muda wa kuwaza juu ya biashara au kazi zako, na watoto nao kwa upande mwingine wanataka muda ambao hutawaza yalio yako bali yaliyo yao tu.

Mara nyingine, watoto hufanya vitu vya kuchekesha, tunachotakiwa ni kucheka nao na sio kuwacheka.  Hii itaepusha kuwaumiza moyo.

4.         Uvumilifu (Patience)
Uvumilivu ni muhimu sana kwa yeyote anayetaka kuwa karibu na watoto.  Watoto hufanya makosa mengi, na pia ni wataratibu katika kufanya mambo maana ujuzi wao bado ni mdogo.  Kwanza ndio wanajifunza kujitawala na kufuata maelekezo na pia wanahitaji kukumbushwa mara kwa mara.  Ni wakati wa kuulizwa maswali mengi na ya marudio, hata yale yasiyo muafaka.

5.         Kuwa na huruma (Compassion)
Huruma kwa watoto huambatana na uvumilivu.  Mtu mwenye huruma ni yule anayetambua pale mwenzake anapokuwa na tatizo au uhitaji na yuko tayari kutoa msaada.  Watoto humwitaji mtu anayewaelewa na kujali mahitaji yao.  Vipo vitu ambavyo vyaweza kuonekana vidogo na vya kawaida kwetu, kumbe kwa watoto ni vikubwa na vyenye kuwaogopesha sana.  Tunategemea huruma na kujali kwako kutaongezeka hasa kwa wale watoto wenye matatizo au uhitaji mkubwa mfano: watoto wenye magonjwa ya kudumu, ulemavu au matatizo ya kifamilia.

6.         Kuwa mtu unayekubali mabadiliko (Be flexible)
Watoto wako tofauti sana na huwezi kuwa tabiri, mara nyingine watataka kitu fulani na mara hubadilika.  Hawana muda wa kufikiri athari au usumbufu wa kubadilika au kubadilisha maamuzi yao.  Kwa sababu ni vigumu kufahamu ni nini kitajiri kwa mtoto baada ya muda mfupi ujao basi ni lazima tuwe tayari kubadilika.  Pasipo hili basi utakuwa na wakati mgumu sana kuwa rafiki wa watoto.

7.         Kuwa Mgunduzi (Be creative)
Mtu mwenye mawazo na fikra za kigunduzi atapata urahisi sana katika kuwa rafiki wa watoto.  Jaribu kuwa mpya kwa watoto kila mara,  sio kila kitu unachofanya kwao kiwe ni kile kile siku zote.  Amsha hamasa yao kwa vitu, mambo au mawazo mapya mawakati wote.  Watoto hawapendi kufanya kitu fulani kwa njia au mfumo uleule kila wakati.

8.         Kuwa mtu wa watu na mpenda watu (Be sociable)
Watoto huwa wanatusoma sana, pale unapojaribu kuwa mwema kwao, kucheka nao na kuwa karibu nao na wakati hauko hivyo kwa wengine ndani au nje ya familia yako unawafanya wasikuelewe na taratibu huanza kukuhofu.
Waruhusu wakuone ukiwa halisi, hususani unapohusiana na wao pamoja na wengine pia.
Wazazi au mzazi anayependa kujitenga na kuwa mpweke hupata shida sana katika kuwafanya watoto kuwa karibu nae.

9.         Maanisha na ujitoe kwao (Be committed)
Wakati unapoamua kufanya kitu na watoto au mtoto, basi maanisha.  Usiwe na vitu vingi wakati mmoja.  Wape nafasi yao na iwe yao peke yao.
Jitoe kufanya vema uwezavyo katika kuhakikisha unawajali na kuwafurahisha watoto.  Watoto pia hufurahi sana pale wanapoona umetoa moyo wako wote kwa ajili yao. Kama umeamua kuanza kitu nao basi malizia, usikiachie katikati.
Kama unajua au kuhisi kwamba hutomaanisha katika lile unalolifanya ukiwa nao basi ni bora uache mpaka pale utakapojiona kuwa utamaanisha.

Maoni 1 :

  1. kuwa karibu na watoto ni jambo muhimu sana maana utafahamu mengi ikiwemo mwenendo wa mtoto ili baadae aishi na jamii vizuri, wazazi na walezi tunapaswa kuwa karibu saana na watoto wetu ili tufahamu miaenendo yao ya hapo baade.

    JibuFuta