Alhamisi, 15 Mei 2014

MAZIWA YA MAMA KWA MTOTO

Umuhimu wa maziwa ya mama kwa mtoto


 Maziwa ya mama ni bora kuliko kitu kingine cho chote kwa kuwa:


·         yana kinga za asili

·         yana virutubisho vyote

·         yanapatikana wakati wote hayahitaji kutayarishwa

·         ni safi na salama

·         yanamfaa mtoto mdogo

·         huleta uhusiano mzuri kati ya mtoto na mama yake

·         kunyonyesha kunasaidia kurudisha tumbo la uzazi la mama katika hali yake ya awali

·         katika miezi sita ya mwanzo mama anayenyonyesha mtoto wake kwa zaidi ya mara kumi kwa siku hapati siku zake za mwezi na hapati mimba mapema.

Maziwa ya kopo siyo sawa na ya binadamu. Ni kazi kuyatayarisha na hayana virutubisho kama maziwa ya mama. Ni chanzo cha magonjwa kama ya kuharisha.




Ukweli kuhusu maziwa ya mama ya mama kwa Mtoto.



 Maziwa haya ni mazuri sana. Maziwa haya kwa lugha ya kizungu yanaitwa Colostrum. Maziwa haya ni mazito, yenye rangi ya njano.

 Ni muhimu mtoto anyonye maziwa haya kwani yamejaa kinga za asili zitakazosaidia kumzuia mtoto asipate magonjwa hasa ya kuharisha na kifua







 


Wakati sahihi wa mama kumnyonyesha mototo wake.

Mama mjamzito anapojifungua tu, cha kumuonjesha mtoto wake si chumvi wala sukari, bali ni maziwa yake mwenyewe. Maziwa ya mama yana kila kitu, yaani chumvi na sukari humo humo. Ni safi, ni fresh, yana usalama, yana viini vya kukinga mwili, yana joto linalomfaa mtoto na hayamletei mtoto kuharisha.



Zawadi kubwa ambayo mama anatakiwa kumpa mtoto wake mchanga ni moja tu, nayo ni maziwa yanayotoka ndani ya ziwa lake mwenyewe. Na ampe ziwa hilo kuanzia mara tu anapozaliwa mtoto. Hakuna sababu yoyote ya kumchelewesha mtoto kunyonya ziwa.






Mtoto anatakiwa aanze kunyonyeshwa maziwa ya mama mara tu anapozaliwa. Hakuna ulazima wowote wa kuchelewesha kitendo cha kumpa mtoto ziwa la mama yake.



Maziwa yako yakichelewa kutoka kwa vile hukumpatia mtoto ziwa mara tu alipozaliwa. Kitendo cha mtoto kunyonya huwa ndiyo msisimko kwa mama kutoa maziwa. Hakuna haja ya kumpa mtoto maji, kwani yatamfanya mtoto ajisikie kutosheka na hivyo asinyonye, na kutonyonya huko ndiko kunakosababisha maziwa yasitoke.



Mtoto mdogo anayenyonya maziwa ya mama tu yaani mtoto aliye na umri chini ya miezi 6 hahitaji maji ya kunywa. Maziwa ya mama yana maji ya kutosha hata wakati wa joto kali. Mtoto mchanga hahitaji maji ya kunywa mpaka afikishe miezi mine hata zaidi.



 Utaalamu wa kunyonyesha mtoto.

Hakuna utaalamu maalum wa kuwanyonyesha watoto wachanga, kila mama anaweza kumnyonyesha mtoto wake. Hakikisha kuwa mtoto anapatiwa ziwa la mama yake mara tu anapozaliwa. Pasiwe na kisingizio cha mama kutokuwa na maziwa kwani kule kunyonyesha ndiko kunakomfanya mama atoe maziwa. 


Mtoto anyonye mara nyingi kiasi atakachopenda mwenyewe, asiwekewe vipimo. Hata wakati wa usiku mtoto asinyimwe kunyonya. Yote hayo ni mambo yanayoweza kuzingatiwa na mama yeyote na hatuwezi kusema kuwa yanahitaji utaalam maalum.


 Ukweli kuhusu kuharibika kwa Maziwa ya mama

Maziwa hayawezi kuharibika yakiwa ndani ya titi la mama. Kama mtoto wako anaharisha labda kuna sababu nyingine lakini siyo maziwa ya mama. Maziwa ya ng’ombe au ya kopo ndiyo yanayoweza kusababisha mtoto kuharisha. 


Vile vile mtoto akiwa na ugonjwa kama vile malaria anaweza kuharisha. Inafaa chanzo cha mtoto kuharisha kitafutwe kwa makini na ikiwezekana ushauri upatikane kutoka kwenye kituo cha afya. Ni muhimu ieleweke kwamba maziwa ya mama pekee hayamfanyi mtoto aharishe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni